SASA rasmi, Yaw Berko amebaki historia ndani ya klabu ya Yanga. Hiyo inafuatia klabu ya St Eloi Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuridhika naye baada ya majadribio.
Katibu wa Yanga, Lawrence Mwalusako ameiambia fzakar.blogspot.com jana kwamba kipa huyo Mghana amefuzu majaribio Lupopo na amesajiliwa moja kwa moja.
Kuondoka kwa Berko, kunatoa nafasi kwa kiungo kutoka DRC, Kabange Twite kusajiliwa katika klabu hiyo ya Jangwani, akiungana na kaka yake, beki Mbuyu Twite. Wachezaji wengine wa kigeni wa Yanga ni kiungo Haruna Niyonzima kutoka Rwanda na washambuliaji Didier Kavumbangu kutoka Burundi na Hamisi Kiiza kutoka Uganda.
Berko alijiunga na Yanga SC mwaka 2009, akitokea Liberty Proffessional ya kwao Ghana, timu ambayo ilimuibua pia Michael Essein na nyota wengine kibao wa Ghana. Aliletwa nchini na kocha wa zamani wa Yanga, Mserbia Kostadin Bozidar Papic aliyewahi kupiga kazi Ghana katika klabu ya Hearts POf Oak.
Alikuwa kipa bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Bara msimu wa 2010/2011 na katika kipindi chake cha kufanya kazi Jangwani, anajivunia kuiwezesha timu kutwaa mataji ya ubingwa wa Bara msimu wa 2010/2011 na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mara mbili mfululizo, 2011 na 2012.
2011 alidaka mechi zote, lakini 2012 alidaka hadi Robo Fainali alipoumia na kumuachia Ally Mustafa ‘Barthez’ aliyedaka hadi ubingwa. Yanga imeridhika na uwezo wa Barthez langoni iliyemsajili kutoka Simba msimu huu na kuamua kuachana na Berko, ambaye alikuwa kipenzi cha wapenzi wa klabu hiyo.
Awali, Yanga ilijifikiria mara mbili kuachana na Berko, kwa kuhofia Barthez angeanza ‘kuwaringia’ kwa kuona amebaki peke yake kipa bora, lakini imepanga kumhamasisha Said Mohamed kuimarisha kiwango chake, vinginevyo atatemwa mwishoni mwa msimu.
Na Yanga imekuwa na ‘jeuri’ ya kumtema Berko baada ya kuona mwakani haitashiriki michuano ya Afrika, zaidi ya Ligi Kuu na jukumu la kwenda kutetea taji lake la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mjini Kigali, Rwanda.
Japokuwa anaondoka, lakini kwa uhodari wake langoni, Berko atabakia kwenye kumbukumbu ya mashabiki wa Yanga.
WASIFU WAKE:
JINA: Yaw Berko
KUZALIWA: Oktoba 13, 1980
ALIPOZALIWA: Accra, Ghana
KLABU ZA AWALI:
Mwaka Klabu
2000-2005: Liberty Professional
2005-2006: Pisico Binh Dịnh F.C. (Vietnam, mkopo)
2006-2009: Liberty Professional
2009- 2012: Yanga SC
2012: St Eloi Lupopo
No comments:
Post a Comment