YANGA imeendelea kuwapa raha mashabiki wake, baada ya kufanikiwa kumaliza vema mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikijishindilia kileleni zaidi, kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji Coastal Union, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Yanga imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa na pointi 29, ikifuatiwa na Azam FC katika nafasi ya pili yenye pointi 24 na Simba SC nafasi ya tatu kwa pointi zao 23.
Hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0. Lililotiwa kimiani na mshambuliaji wake wa kimataifa wa Burundi, Didier Kavumbangu dakika ya 28, kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na kiungo Simon Msuva.
Kipindi cha pili, Yanga walirejea na moto wao tena na iliwachukua dakika 17 tu kuandika bao la pili, mfungaji Mganda Hamisi Kiiza ‘Diego’ aliyeuwahi mpira ambao aliuokosa beki wa Coastal, Mbwana Hamisi na kuutumbukiza nyavuni kiulaini.
Yanga SC; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Nurdin Bakari, Frank Domayo, Simon Msuva, Hamisi Kiiza, Haruna Niyonzima na Didier Kavumbangu/Said Bahanuzi.
Coastal Union; Juma Mpongo, Ismail Amour Khamis, Juma Jabu, Jamal Macherenga/Othman Omar Tamim, Mbwana Hamisi, Jerry Santo, Soud Mohamed, Razack Khalfan, Daniel Lyanga, Atupele Green/Lameck Dayton na Suleiman Kassim ‘Selembe’.
No comments:
Post a Comment