MAMBO yameiva Yanga- matumaini ya wapenzi wa klabu hiyo kushuhudia klabu yao ikiwa na Uwanja mpya wa kisasa yameanza kuonyesha dalili za kutimia, kufuatia uongozi wa klabu hiyo kusaini makubaliano ya awali na Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group iliyojenga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Kaunda.Mwenyekiti wa mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati, Alhaj Yussuf Mehboob Manji leo amesaini makubaliano na Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo, David Zhang, makao makuu ya klabu hiyo, makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga, Dar es Salaam.Katika makubaliano hayo, ujenzi huo wa Uwanja utakaokuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 30,000 hadi 40,000 utaanza rasmi Juni mwakani.Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa kusaini makubaliano hayo leo mchana, Alhaj Manji alisema kwamba wanfurahi kuanza safari ya ujenzi wa Uwanja wao na anaamini huo ni mwanzo wa mzuri wa mipango yao ya kuifanya Yanga ijitegemee kiuchumi.Katika hatua nyingine, Manji amesema kwamba katika mipango yao ya kuifanya Yanga ijimudu kiuchumi, wanafikiria kulikarabati pia jengo dogo la klabu hiyo, liliopo Mtaa wa Mafia.Alhaj Manji alisema Jumatatu kampuni hiyo ya ujenzi kutoka China, ambayo ndiyo iliyojenga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itachukua vipimo kwenye Uwanja wa Kaunda na Uongozi wa Yanga kuliwasilisha suala la ujenzi huo kwenye Mkutano Mkuu wa Wanachama wa klabu hiyo, Desemba 8, mwaka huu.Alisema baadhi ya fedha kwa ajili ya uwanja huo wa kisasa watakapo benki na gharama nyingine zitatokana na michango ya wanachama baada ya kuwa wamepata gharama nzima za ujenzi za uwanja huo.Meneja Mkuu wa Kampuni ya Beijing Cobnstruction Engineering Group alisema wanafurahia kufikia makubaliano ya awali ya ujenzi wa uwanja na klabu ya Yanga.Alisema wao ndio walijenga Uwanja wa Taifa na viwango vya ujenzi vya uwanja huo vilisifiwa na timu ya taifa ya Brazil iliyokuja kucheza mechi ya kirafiki na Tanzania mwaka 2010 ikiwa njiani kuelekea Afrika Kusini ambako fainali za kombe la Dunia zilifanyika.
No comments:
Post a Comment