habari

MATANGAO

Sunday, November 11, 2012



YANGA imeendelea kuwapa raha mashabiki wake, baada ya kufanikiwa kumaliza vema mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikijishindilia kileleni zaidi, kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji Coastal Union, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Yanga imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa na pointi 29, ikifuatiwa na Azam FC katika nafasi ya pili yenye pointi 24 na Simba SC nafasi ya tatu kwa pointi zao 23.
Hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0. Lililotiwa kimiani na mshambuliaji wake wa kimataifa wa Burundi, Didier Kavumbangu dakika ya 28, kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na kiungo Simon Msuva.
Kipindi cha pili, Yanga walirejea na moto wao tena na iliwachukua dakika 17 tu kuandika bao la pili, mfungaji Mganda Hamisi Kiiza ‘Diego’ aliyeuwahi mpira ambao aliuokosa beki wa Coastal, Mbwana Hamisi na kuutumbukiza nyavuni kiulaini.
Yanga SC; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Nurdin Bakari, Frank Domayo, Simon Msuva, Hamisi Kiiza, Haruna Niyonzima na Didier Kavumbangu/Said Bahanuzi.
Coastal Union; Juma Mpongo, Ismail Amour Khamis, Juma Jabu, Jamal Macherenga/Othman Omar Tamim, Mbwana Hamisi, Jerry Santo, Soud Mohamed, Razack Khalfan, Daniel Lyanga, Atupele Green/Lameck Dayton na Suleiman Kassim ‘Selembe’.

Friday, November 9, 2012

CHAGUENIKIKOSI KITAKACHO SHINDA MECHI ZA TANZANIA.
SIMBA SPORT CLUB.
YOUNG AFRICAN SPORT CLUB

CHAGUENIKIKOSI KITAKACHO SHINDA MECHI ZA TANZANIA.
AZAM FOOTBALL CLUB
JKT MGAMBO
MTIBWA SUGAR.
COASTAL UNION.

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania .


SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania limeteua wadau 10 kwa ajili ya kusaidia timu ya taifa ya vijana walio na umri chini ya miaka 17, Serengeti Boys itakayopambana na Congo (Brazaville) katika mechi ya raundi ya tatu ya michuano ya awali ya Mataifa ya Afrika.
Uteuzi huo umefanywa na Rais wa TFF, Leodegar Tenga baada ya Kamati ya Vijana ya TFF kufanya kikao chake kujadili kwa umakini ushiriki wa timu hiyo na kupeleka mapendekezo yake kwa rais huyo wa shirikisho.
Kutokana na umuhimu wa mechi hiyo itakayoamua timu itakayofuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, TFF imeona umuhimu wa kuwa na kamati ambayo itakuwa na majukumu mawili makubwa ambayo ni:
1. Kuhamasisha vijana waone umuhimu na kuwa na ari ya kushinda mechi hiyo
2. Kuhamasisha umma uone umuhimu wa mechi hiyo na hivyo kuisaidia iweze kufuzu.
Walioteuliwa kuunda kamati hiyo ni:1. Ridhiwani Kikwete Mwenyekiti2. Ahmed Seif (Magari) Mjumbe3. Nassoro Bin Slum Mjumbe4. Henry Tandau Katibu5. Ahmed Mgoyi Mjumbe6. Aboubakar Bakhresa Mjumbe7. Angetile Osiah Mjumbe8. Kassim Dewji Mjumbe9. Abdallah Bin Kleb Mjumbe10. Salim Said Mjumbe
Baada ya kuvuka raundi mbili za kwanza bila ya kucheza mechi kutokana na wapinzani wake kujitoa, timu ya Serengeti Boys inahitaji kufanya kila iwezalo kuweza kuiondoa Congo kwenye mashindano hayo na kuweka rekodi ya kufuzu kucheza fainali hizo za Afrika ambazo pia zitatoa wawakilishi wa Afrika kwenye mashindano ya Kombe la Dunia. 
Mechi za kwanza za raundi ya tatu zitachezwa kati ya Novemba 16 na 18, 2012 na mechi za marudiano zitachezwa kuanzia Novemba 30, 2012 hadi Desemba 2, 2012

Tuesday, November 6, 2012


KIPA wa zamani wa Simba na aliyekuwa kocha wa makipa wa timu hiyo, Iddi Pazi ‘Father’ amesema kwamba uwezo wa kipa namba moja wa sasa klabu hiyo umeshuka na tiba yake anaijua.“Kaseja uwezo umeshuka kidogo, kwa sababu daktari wake sipo pale, Simba wakinirudisha kazini, Kaseja atafufua makali yake na atakuwa hafungiki kwa urahisi,”alisema Pazi.Pazi ameushauri uongozi wa Simba umerejeshe kazini ili aokoe kipaji cha kipa huyo bora, miongoni mwa walinda milango bora kuwahi kutokea Tanzania.Kwa sasa, kocha wa makipa wa Simba ni kipa mwingine wa zamani wa Simba, James Kisaka ambaye alipewa kazi hiyo baada ya Pazi kwenda Oman. Lakini kwa sasa Pazi amemaliza mkataba wake Oman na yupo nyumbani kwake, Majumba Sita, Ukonga, Dar es Salaam.Katika mechi 12, Kaseja amefungwa mabao 10 kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzanoia Bara msimu huu, kitu ambacho si kawaida yake katika misimu iliyotangulia, ingawa hiyo inaelezwa inachangiwa hata na ubutu wa safu ya ulinzi ya sasa wa timu hiyo.Lakini pia, kocha Mserbia wa Simba SC, Profesa Milovan Cirkovick naye anadaiwa kuchangia matokeo mabaya na habari zinasema anaweza kutimuliwa wakati wowote kwenye klabu hiyo, kufuatia kutofautiana na uongozi wa klabu hiyo.Uongozi wa Simba unamtuhumu Mserbia huyo kwamba ni mbishi hashauriki na hilo limekuwa likiigharimu timu katika michezo yake ya karibuni ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.“Huyu jamaa tumemvumilia sana, mimi sina hamu naye tena, sijui wenzangu. Anapanga kikosi ovyo na ndiyo chanzo cha matokeo haya mabaya,”alisema kiongozi mmoja wa Simba. Lakini kwa upande mwingine, inadaiwa matokeo haya mabaya ya Simba ni matokeo ya mgomo wa wachezaji wakishinikiza wachezaji wenzao waliosimamishwa Haruna Moshi ‘Boban’ na Juma Nyosso warejeshwe kikosini.Zaidi Boban, wachezaji wanadaiwa kumpenda sana kutokana na roho yake safi ya kibinadamu na upendo mkubwa kwa wenzake.Boban ndiye mchezaji pekee aliyejitolea kuusindikiza nyumbani kwao, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mwili wa marehemu Patrick Muteesa Mafisango, kiungo wa Simba aliyefariki dunia Mei mwaka huu kwa ajali ya gari.Simba SC juzi ilifungwa mechi ya kwanza ya Ligi Kuu mabao 2-0 na Mtibwa Sugar, Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, mabao ya Said Mkopo na Hussein Javu.Simba inabaki na pointi zake 23, baada ya kucheza mechi 12, ikiipisha kileleni Yanga yenye pointi 26 sasa. Simba itamaliza mzunguko wa kwanza wa ligi kwa kumenyana 

Sunday, November 4, 2012



YANGA SC imepanda kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuifunga Azam FC mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo, unaifanya Yanga iongoze Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 26, ikiwa imebakiza mechi moja ya mzunguko wa kwanza dhidi ya Caostal Union mjini Tanga, ikifuatiwa na Simba SC yenye pointi 23, ambayo leo imefungwa 2-0 na Mtibwa Sugar mjini Morogoro.
Hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Didier Kvumbangu aliyeunganisha krosi ya Simon Msuva kutoka wingi ya kulia dakika ya tisa.
Katika kipindi hicho, Yanga timu zote zilicheza kwa kiwango sawa, isipokuwa Yanga ndiyo iliyokuwa na mashambulizi ya kutisha zaidi.
Mabeki wa Yanga walimdhibiti vema mshambuliaji hatari wa Azam, John Bocco ‘Adebayor’ na kitendo cha kocha Mholanzi, Ernie Brandts kupanga viungo wawili wakabaji, Athumani Iddi ‘Chuji’ na Frank Domayo viliisaidia timu hiyo kuwabana Azam  katikati ya Uwanja.
Kipindi cha pili, Yanga walirudi vizuri zaidi na kuifunika kabisa Azam, ambayo leo hakika ilimsononesha kocha wake, Muingereza Stewart Hall.
Mganda, Hamisi Kiiza ‘Diego’ aliifungia Yanga bao la pili dakika ya 68, akiunganisha krosi ya Athumani Iddi ‘Chuji’ kutoka wingi ya kulia.
Baada ya bao hilo, Kiiza alivua jezi yake na kubaki na fulana ya njano yenye maandishi; Rest In Peace Mafisango, I miss you So much my brother, maana yake akimuenzi aliyekuwa kiungo wa Simba, Patrick Mutesa Mafisango aliyefariki dunia kwa ajali ya gari Mei mwaka huu akiwa mchezaji wa klabu hiyo.
Kwa ujumla Yanga imebadilika mno kiuchezaji na sasa wanacheza kwa kuonana, kupeana pasi za uhakika ndefu na fupi, kuwabana wapinzani na pia bila kuchoka muda wa mchezo.
Kikosi cha Yanga SC leo kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo, Simon Msuva/Paul Ngalema, Hamisi Kiiza, Haruna Niyonzima na Didier Kavumbangu.
Azam FC; Mwadini Ally, Erasto Nyoni/Samir Hajji Nuhu, Ibrahim Shikanda, Aggrey Morris na Said Mourad, Jabir Aziz/Ibrahim Mwaipopo, Kipre Balou, Khamis Mcha ‘Vialli’/Abdi Kassim ‘Babbi’, Salum Abubakar, John Bocco na  Kipre Tcheche.
Katika mchezo wa utangulizi, Yanga B imewafunga Azam B, maarufu kama Azam Academy mabao 2-0. Mabao ya Yanga B yalifungwa na Joseph Banda na Claver Charles kipindi cha kwanza.
Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo, Mtibwa Sugar iliichapa mabao 2-0 Simba SC, Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, mabao ya Said Mkopo na Hussein Javu.
Simba inabaki na pointi zake 23, baada ya kucheza mechi 12, ikiipisha kileleni Yanga yenye pointi 26 sasa. Simba itamaliza mzunguko wa kwanza wa ligi kwa kumenyana na Toto African uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 

Saturday, October 27, 2012


PICHA ZA SIMBA SPORT CLUB NA AZAM FC, LEO MECHI ILI KUWA NGUMU KIDOGO KWA AZAMFC  WAMEFUNGWA 3-1 ASAHIVI SIMBA SPORT CLUB IPO JUU SANA KWA POINT.NA YANGA SPORT CLUB WAMEFANIKIWA KUWA FUNGA JKT OLJORO BAO 1-0.


Monday, October 8, 2012


BAO pekee la Themi Felix katika dakika ya 67, jioni ya leo limewapa Kagera Sugar ushindi wa 1-0 dhidi ya Yanga SC, kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Felix aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mnigeria, Enyinna Darlington kwa kumtungua bao hilo, kipa Mghana wa Yanga, Yaw Berko, ameendeleza rekodi yake kuvifunga vigogo, Simba na Yanga katika Uwanja huo.
Hiyo inakuwa mechi ya pili Yanga kufungwa ndani ya mechi sita walizocheza hadi sasa na mbili wametoka sare- maana yake inabaki na pointi zake nane na kuzidi kujipunguzia matumaini ya ubingwa msimu huu, ikiwa sasa inazidiwa pointi nane na vinara wa ligi hiyo Simba SC.
Aidha, hii ni mechi ya pili Yanga inacheza chini ya kocha wake mpya, Mholanzi Ernie Blandts aliyerithi mikoba ya Mbelgiji, Tom Saintfiet na katika mechi hizo mbili ameambulia pointi moja kutokana na sare dhidi ya Simba Jumatano.
Kwa ujumla Yanga haijashinda hata mechi moja ya ugenini kati ya tatu ilizocheza hadi sasa, ilitoka 0-0 na Prisons, ikafungwa 3-0 na Mtibwa na leo imechapwa 1-0 na Kagera Sugar, wakati Alhamisi itacheza na Toto African mjini Mwanza.
Katika mechi hiyo, Yanga ilipata pigo dakika ya 23 baada ya mshambuliaji wake mahiri na tegemeo, Said Bahanuzi ‘Spider Man’ kuchanika nyama za paja dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete.
Tangu ajiunge na Yanga akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, leo Bahanuzi amecheza mechi ya 13 kwa dakika hizo 23 na ameifungia timu hiyo jumla ya mabao 12, matatu kati ya hayo kwa penalti.
Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Omar Juma kutoka Mwanza, aliyesaidiwa na Dominick Nyamsana wa Dodoma na Hassan Zani wa Arusha, kikosi cha Yanga kilikuwa; Yaw Berko, Juma Abdul, Stefano Mwasyika/nurdin, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Athumani Iddi ‘Chuji’, Nizar Khalfan, Frank Domayo, Didier Kavumbangu, Said Bahanuzi/Jerry Tegete na Haruna Niyonzima.
Kagera; Andrew Ntala, Jumanne Nade, Salum Kanoni, Amandus Nesta, Benjamin Effe, Malegsesi Mwangwa, Daudi Jumanne, George Kavilla, Enyinna Darlington/Themi Felix, Shijja Mkinna na Wilfred Emmeh/Paul Ngway.
Katika mechi zilizochezwa jana, Simba SC ilizidi kujiimarisha kileleni kufuatia ushindi wa mabao 4-1 ilioupata kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha, ambayo ilimaliza pungufu ya wachezaji wawili baada ya kipa wake Shaibu Issa na mshambuliaji Meshack Nyambele kutolewa kwa kadi nyekundu kipindi cha pili.
Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Amon Paul wa Mara, aliyesaidiwa na Anold Bugabo wa Singida na Charles Simon wa Dodoma, hadi mapumziko Simba walikuwa tayari mbele kwa mabao 2-1, mabao yake yote yakitiwa kimiani na kiungo Amri Ramadhan Kiemba katika dakika za 16 na 44, wakati la Oljoro lilifungwa na Paul Nonga dakika ya 29.
Kiemba alifunga bao la kwanza akiunganisha krosi pasi ya Christopher Edward, wakati bao la pili lilitokana na krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’, yote kutokana na mashambulizi ya upande wa kulia.
Ilikuwa rahisi kwa Kiemba kufunga mabao yote akiwa kwenye eneo la hatari, kutokana na mabeki wa Oljoro kumuwekea ulinzi zaidi Felix Sunzu.
Nonga naye alifunga bao lake baada ya kupewa pasi ndefu na kumpiga chenga kipa na Nahodha wa Simba, Juma Kaseja upande wa kulia mwa Uwanja na kuutumbukiza mpira nyavuni kiulaini.
Bao hilo lilitokana na beki Paul Ngalema kupokonywa mpira wakati amepanda kusaidia mashambulizi na Oljoro wakafanya shambulizi la haraka.
Kipindi cha pili Simba walirudi vizuri zaidi uwanjani na kuuteka zaidi mchezo- jambo ambalo liliwafanya Oljoro wawapunguze kasi kwa kuwachezea rafu. Hilo liliwagharimu kupoteza wachezaji wao wawili kabla ya filimbi ya mwisho na kufungwa mabao mawili zaidi.
Dakika ya 83 Mganda Emanuel Okwi aliifungia Simba bao la tatu na katika dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 90 za mchezo, Okwi akiwa anaelekea kufunga tena, alikwatuliwa na kipa wa Oljoro Shaibu Issa na refa akaamuru penalti sambamba na kumtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja mlinda mlango huyo.
Awali ya hapo, Oljoro ilimpoteza mchezaji mwingine, Nyambele dakika ya 78, ambaye alionyeshwa njano ya pili kwa rafu aliyomchezea Jonas Mkude. Nahodha Kaseja alitaka kwenda kupiga, lakini akazuiwa na Felix Mumba Sunzu akaenda kufunga bao la nne kwa mkwaju wa penalti.
Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 16 baada ya kucheza mechi sita, hivyo kuendelea kuongoza Ligi Kuu, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 13, ingawa imecheza mechi tano.
Katika mechi nyingine za jana, Mgambo imepata ushindi wake wa kwanza baada ya kuichapa Polisi Morogoro 1-0, wakati Toto African imeichapa JKT Ruvu 2-1 na Prisons imelazimishwa sare ya bila kufungana na Mtibwa Sugar.