KOCHA Mkuu
wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet amewaomba radhi mashabiki wa Yanga kwa sare ya
Jumamosi kwenye Uwanja wa Sokoine na amesema kesho anapeleka wachezaji 18
Morogoro kwa ajili ya mechi ya pili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi
ya Mtibwa Sugar, akiwa ana matumaini makubwa ya
ushindi.
Saintfiet
ameiambia http://ramadhanabubakar.blogspot.com/ leo kwamba sababu nyingi zilichangia Yanga
kutocheza kwa ubora wake Mbeya, ikiwemo hoteli mbaya na chakula kibaya na kwa
ujumla alisema hawakuwa vizuri kabla ya mechi hiyo.
“Mimi kwa
mfano sijaoga siku mbili, kwa kweli tulikuwa katika mazingira magumu na
wapinzani wetu walicheza soka ya kuudhi tangu mwanzo, kupoteza muda, na marefa
hawakuchukua hatua, tulipoteza nafasi kupitia kwa Kiiza (Hamisi) na Msuva
(Simon), siwezi kulaumu mchezaji wangu yeyote, lakini hiyo ndiyo hali
halisi,”alisema Saintfiet.
Alisema
kesho asubuhi timu itafanya mazoezi kwenye Uwanja wa sekondari ya Loyola,
Mabibo, Dar es Salaam na saa 8:00 mchana watasafiri kwa njia ya barabaraba
kwenda Morogoro ambako wakifika watatafuta hoteli nzuri
mapema.
Alisema
anajua hata Uwanja wa huko, Jamhuri si mzuri na mechi itakuwa ngumu kwa sababu
Mtibwa Sugar nao walitoka sare ya bila kufungana na Polisi katika mchezo wao wa
kwanza Jumamosi na anaiheshimu timu hiyo kama moja ya timu tano kubwa Tanzania,
pamoja na Simba, Azam na Coastal Union.
“Lakini
pamoja na kwamba Simba wamependelewa kupangiwa ratiba ya kuanza kucheza nyumbani
mechi tano mfululiuzo, nakuambia Mei mwaka 2013 Yanga ndio itavishwa taji la
ubingwa wa Ligi Kuu, acha wafurahie sasa hivi, watalia mwisho,”alisema Mtakatifu
Tom.
Kuhusu
wachezaji 18 anaokwenda nao Morogoro, Mtakatifu Tom alisema atawataja baada ya
mazoezi ya kesho na hiyo inaonekana ni kwa sababu ya kufuatilia hali za
wachezaji ambao kwa sasa hawako vizuri, akiwemo kiungo Haruna
Niyonzima.
Wachezaji
aliokwenda nao Mbeya walikuwa ni makipa; Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barthez’,
mabeki Shadrack Nsajigwa, Juma abdul, Godfrey Taita, Mbuyu Twite, Kevin Yondan,
Nadir Haroub ‘Cannavaro’, David Luhende, Oscar Joshua na Stefano
Mwasyika.
Aliwataja
viungo ni Athumani Iddi ‘Chuji’, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Rashid Gumbo,
Nizar khalfan, Shamte Ally na Simon Msuva, wakati washambuliaji ni Jerry Tegete,
Didier Kavumbangu, Said Bahanuzi na Hamisi Kiiza, wakati waliobaki walikuwa ni
kipa Said Mohamed, mabeki Ladislaus Mbogo, Job Ibrahim, viungo Juma Seif
‘Kijiko’, Salum Telela, Omega Seme, Nurdin Bakari, Idrisa Assega na Issa Ngao wa
Yanga B, anayekomazwa kikosi cha kwanza.
No comments:
Post a Comment