AZAM FC tayari wako mjini Mwanza na asubuhi hii wanafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Ualimu (TTC), Butimba mjini humo kujiandaa na mechi yao ya pili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Toto African, Uwanja wa Kirumba mjini humo.
Azam iliyoanza vema ligi hiyo kwa ushindi wa 1-0 kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, bao pekee la Abdulhalim Humud dhidi ya wenyeji Kagera Sugar, imepania kuondoka na pointi zote sita katika mechi zake zote mbili za Kanda ya Ziwa.
Aidha, mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi kesho watafanya mazoezi kwenye Uwanja Kirumba, ili kuuzoea kabla ya mchezo wa keshokutwa, ambao unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua.
Toto Africans itahitaji ushindi kwenye mchezo huo, ili kurejesha imani kwa mashabiki wake baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na JKT Oljoro, katika mchezo wa ufunguzi Jumamosi.
Kuelekea mchezo huo, Mserbia anayeinoa Azam, Boris Bunjak ameomba marefa wachezeshe kwa haki, kwani anaamini vijana wake wanaweza kushinda pale tu sheria 17 zinapotekelezwa uwanjani na si vinginevyo.
Kocha huyo aliwalalamikiwa marefa waliochezesha mechi yao ya Ngao ya Jamii na Simba kwamba waliwabeba mno wapinzani wake, hata wakatoka nyuma kwa 2-0 na kushinda 3-2.
Kwa upande wake, Kocha wa Toto, John Tegete amesema kwamba baada ya kulazimishwa sare na Oljoro, Jumatano watapigana kufa na kupona ili kushinda mechi ya kwanza ya Ligi Kuu.
“Sare ya juzi kwa kweli hatukuitarajia, tulicheza vizuri, tulipata nafasi nyingi tukapoteza, lakini kwa siku mbili hizi tutafanyia kazi makosa yetu na Jumatano tunaomba mashabiki waje kwa wingi kushuhudia mabadiliko, tunawaahidi ushindi,”alisema baba huyo wa mshambuliaji wa Yanga, Jerry Tegete.
No comments:
Post a Comment