habari

MATANGAO

Wednesday, December 19, 2012


AZAM FC imefanikiwa kuingia Nusu Fainali ya Kombe la Hisani mjini hapa, baada ya kuilaza Real de Kinshasa kwenye Uwanja wa Martyrs, katika mchezo maalum wa kutafuta timu ya kutinga Nusu ya michuano hiyo inayoandaliwa na FECOFA, Shirikisho la Soka DRC.
Shukrani kwao, washambuliaji Gaudence Mwaikimba na Seif Abdallah waliofunga mabao hayo, moja kila kipindi.
Ikiongezewa nguvu na nyota wake watatu, Kipre Tchetche, Kipre Balou raia wa Ivory Coast na Mkenya, Joackins Atudo waliochelewa mechi mbili za awali, Azam leo ilitawala mchezo na kama si rafu za wapinzani wao, ingevuna ushindi mtamu.
Hadi mapumziko, tayari Azam walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na Mwaikimba dakika ya 21, ambaye aliunganisha pasi nzuri ya Kipre kutoka wingi ya kushoto.
Hilo linakuwa bao la pili kwa Mwaikimba, mshambuliaji wa zamani wa Kahama United, Ashanti United, Yanga, Prisons na Kagera Sugar katika mechi tatu za mashindano haya alizocheza, awali alifunga katika sare ya 1-1 na Dragons.
Kipre Tchetche alilazimika kutoka nje ya Uwanja dakika ya 43 kutokana na rafu za wachezaji wa Real, nafasi yake ikichukuliwa na Samih Hajji Nuhu.
Real walikuwa wakipiga kiatu haswa na kiungo Waziri Salum aliungana na Kipre Tchetche kuuacha Uwanja kabla ya filimbi ya kuugawa mchezo, ingawa nafasi yake ilichukuliwa na Uhuru Suleiman dakika ya kwanza ya kipindi cha pili.
Awali ya hapo, refa Madila Achille alimtoa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 43 beki Muipalayi Igongo kwa kumchezea rafu mbaya Gaudence Mwaikimba, ambayo chupuchupu naye imtoe nje, kiasi cha kulazimika kumalizia mechi akichechemea.
Kipindi cha pili, Azam waliendelea kuwafundisha soka Real na katika dakika ya 73, kazi nzuri ya Mwaikimba ilisaidia kupatikana bao la pili. Mpira mrefu uliopigwa na kipa Mwadini Ally, Mwaikimba aliumiliki vema, akatoa pasi pembeni kushoto kwa Hajji Nuhu ambaye aliingia ndani kidogo na kukata krosi maridadi iliyounganishwa kimiani na Seif.
Humphrey Mieno alikuwa mwathirika mwingine wa rafu za Real, baada ya kulazimika kutoka nje dakika ya 77, akimpisha Abdi Kassim ‘Babbi’.
Azam walionekana kuridhika baada ya kuwa wanaongoza mabao 2-0 na wakafanya uzembe uliowapa bao la kufutia machozi Real, lililofungwa na Bisole Panzu dakika ya 78.
Baada ya mechi hiyo, kocha wa Azam, Muingereza Stewart Hall aliwapongeza vijana wake, lakini akasema anakabiliwa na wakati mgumu katika hatua inayofuata kutokana na wachezaji wake wanne kuumia leo.
Kocha wa Real, Sandra Makombele aliwasifu Azam ni timu nzuri na akasema anakubali matokeo, ingawa aliwapiga kijembe. “Wachezaji wangu wana mazoezi mengi, Azam hawana mazeozi, wakiguswa kidogo wanaumia, hakukuwa na rafu, ule ni mchezo wa nguvu kama Ulaya, kocha wao inabidi awape mazoezi mengi wawe wagumu,”alisema mwanamama huyo.
Katika mechi zake mbili za awali za Kundi B, Azam ilitoka 1-1 na Dragons na ikafungwa 2-0 na Shark FC.
Azam ilicheza mechi zote mbili bila makocha wake wote wawili, Waingereza Stewart Hall na Msaidizi wake, Kali Ongala ambao walibaki Nairobi, Kenya pamoja na Daktari Mjerumani Paulo Gomez na wachezaji Kipre Balou na Kipre Tcheche raia wa Ivory Coast, kutokana na kukosa viza za kuingia DRC.
Watano hao, waliwasili mjini Kinshasa jana na beki Joackins Atudo naye amewasili leo na wote wameshiriiki mchezo wa leo kikamilifu.
Nusu Fainali zitachezwa Desemba 25 wakati Desemba 26 itakuwa Fainali na mechi ya kusaka mshindi wa tatu.
Kikosi cha Azam leo kilikuwa; Mwadini Ally, Himid Mao, Waziri Salum/Uhuru Suleiman dk46, Omar Mtaki/Joackins Atudo dk46, David Mwantika, Jabir Aziz, Kipre Balou/Malika Ndeule dk85, Seif Abdallah, Kipre Tchetche/Samih Hajji dk43, Humphrey Mieno/Abdi Kassim dk77 na Gaudence Mwaikimba.

No comments:

Post a Comment