habari

MATANGAO

Thursday, January 3, 2013


KOCHA mpya wa mabingwa wa Bara, Simba SC ya Dar es Salaam, Mfaransa Patrick Liewig amerufahishiwa na uwezo wa wachezaji wa timu hiyo baada ya kuwashuhudia jana wakiwachapa mabingwa wa Zanzibar, Jamhuri ya Pemba mabao 4-2 kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.
Hata hivyo, kocha huyo wa zamani wa Akademi ya PSG ya Ufaransa, amesema kwamba timu ina mapungufu ya kufanyia kazi, kubwa zaidi ni kucheza kama timu.
“Wachezaji wamecheza vizuri, ila kuna mapungufu madogo madogo ya kufanyia kazi na ndiyo maana walifungwa yale mabao mawili, ni mambo madogo, Simba ni timu kubwa huwezi kuifananisha nah ii (Jamhuri),”alisema.
Liewig jana alikuwa jukwaani wakati wote wa mchezo huo, ameketi na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya klabu hiyo, Daniel Manembe akifuatilia mchezo huo.
Mfaransa huyo alitua Dar es Salaam Jumatatu na Jumanne akasaini mkataba wa miezi 18 wa kuifundisha timu hiyo kabla ya jana kuja kuungana na timu visiwani Zanzibar.
Baada ya kusaini mkataba juzi, Liewig alisema kwamba lengo lake ni kuifikisha klabu hiyo katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu na anaamini hilo linawezekana kwa kuwa timu ina wachezaji wazuri.
Alisema kwamba ana imani Simba ni timu nzuri, kwa sababu katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kilichoifunga 1-0 Zambia, kulikuwa kuna wachezaji wengi wa Simba SC.
“Zambia ni timu nzuri, ni mabingwa wa Afrika, kama Tanzania iliifunga Zambia ikiwa na wachezaji wengi wa Simba, sioni kwa nini tusifike Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa,”alisema Liewig.
“Nimeambiwa pia kuna Kombe la Kagame (Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati) Rwanda, tutakwenda, pamoja na yote, nitashughulikia pia na program ya vijana, lazima tuibue vipaji kutoka chini,”alisema.
Simba SC itaanza na Recreativo de Libolo ya Angola, katika Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Februari 17 hadi 19 na kurudiana nayo kati ya Machi 2 na 4, mwakani.
Liewig ni kocha wa zamani wa Akademi ya Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa, ASEC Mimosas ya Ivory Coast na Club Africain ya Tunisia, ambaye ana Stashahada ya Juu ya ukocha na Shahada ya tatu ya ualimu wa soka ya vijana aliyotunukiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Ufaransa, Gerard Houiller, anatarajiwa kwenda Zanzibar kesho.
Liewig pia amehudhuria kozi za ufundishaji mazoezi ya viungo Juni mwaka 1999 katika Chuo Kikuu cha Dijon.
Kwa upande wa uzoefu, Liewig alifanya kazi PSG kuanzia mwaka 1989 hadi 1999 kama Kocha Mkuu wa akademi na kuna wakati alikuwa akishirikishwa pia katika programu za timu A, ingawa majukumu yake zaidi yalikuwa ni kwa Under 20, Under 18 aliowawezesha kutwaa Kombe la French Junior Gambardella na Under 16.
Kuanzia mwaka 1989 hadi 1990: alikuwa Meneja Mkuu wa Tomislav IVIC, 1990 hadi 1991 alikuwa Msaidizi wa Henri Michel, 1991 hadi 1994 alikuwa Msaidizi wa Artur Jorge, 1994 hadi 1996 alikuwa Msaidizi wa Luis Fernandez, 1996 hadi 1998: alikuwa Msaidizi wa Ricardo Gomez, 1998 hadi 1999 alikuwa Msaidizi wa Alain Giresse.
Liewig pia alifundisha Al Wahda FC ya Abu Dhabi kuanzia 1999 hadi 2001, ambayo aliipa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na Kombe la Ligi.
Januari mwaka 2003 alikuwa Msimamizi wa Chama cha Soka UAE katika fainali za Afrika za U20 nchini Burkina Faso.
Kuanzia mwaka 2004 hadi 2009 alikuwa Kocha wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast aliyoipa mataji matatu ya Ligi Kuu ya nchini humo mfululizo, 2004, 2005 na 2006, Super Cup ya nchini humo 2005, 2007, 2008 na 2009 na akaiwezesha kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mara tatu, mara moja akiifikisha Nusu Fainali.
Amekuwa Kocha bora wa Ivory Coast miaka mitatu mfululizo, 2004, 2005 na 2006 na tangu Septemba mwaka jana hadi Juni mwaka huu, alikuwa kocha wa Club Africain ya Tunisia

No comments:

Post a Comment