habari

MATANGAO

Monday, September 17, 2012

Siku ya jumamosi tarehe 15, mwezi wa tisa mwaka 2012, soka la Tanzania lilitengeneza historia nyingine mbaya.
Ilikuwa ni siku ya ufunguzi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania bara na timu mbalimbali zilikuwa viwanjani kutupa karata zao za mwanzo kabisa ndani ya msimu mpya wa 2012/13. Miongoni mwa mechi zilizokuwa zichezwe siku hiyo ilikuwa ni mechi kati mabingwa watetezi Simba na African Lyon zote kutoka Jijini Dar es Salaam.

Mapema asubuhi ya siku hiyo kulikuwa na mkutano wa waaandishi wa habari ulioitishwa na African Lyon na kampuni ya mawasiliano ya  simu za mkononi ya Zantel ambao siku hiyo walikuwa wameamua kutangaza rasmi muunganiko wao wa kibiashara - ambapo klabu hiyo itakuwa ikidhaminiwa na Zantel kwa muda wa miaka mitatu.

Hii ilikuwa habari nzuri kwa wapenda maendeleo ya soka wa Tanzania ikizingatiwa ni vilabu vichache tu ndivyo ambavyo vilikuwa vina udhamini hivyo kuwa na nguvu kuliko vilabu vingine na mwisho wa siku ushindani wenye tija katika kuukuza mpira ukawa sio mkubwa. Hivyo kuingia kwa Zantel kuidhamini African Lyon kulimaanisha kutaipa nguvu klabu hiyo kuweza kupambana na vilabu vingine vyenye fedha na nguvu kama Simba, Yanga, Azam, Mtibwa na nyinginezo.

Muda ukapita na saa ya kwenda uwanjani ikafika, timu zote zikawasili uwanjani na kuanza maandalizi ya mchezo. Kama ilivyo ada, kutokana udhamini ulivyo Simba ambao udhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro walikuwa na jezi zao zenye nembo ya mdhamini wao na wakaenda kuweka mabango yao ya mdhamini wao pembeni mwa uwanja - African Lyon nao baada ya kuwa wameshakamilisha udhamini wa Zantel, walikuwa na jezi zao zenye nembo ya mdhamini wao na pia wakaenda kuweka mabango uwanjani kama ilivyokuwa kwa Simba. Lakini cha ajabu ikatolewa amri kutoka TFF kwamba African Lyon hawatoruhusiwa kuvaa jezi za mdhamini wao mpya na mabango yao yakatolewa dimbani - huku sababu ikitoka kwamba hairuhusiwi kwa timu binafsi inayoshiriki ligi kuu kuwa na udhamini wa kampuni ya simu tofauti na Vodacom ambao ndio wadhamini wakuu wa ligi kuu. Kwa maana hiyo African Lyon iliwabidi watafute jezi nyingine zisizo na nembo ya mdhamini wao mpya na mabango yao yote yakatolewa ndani ya uwanja wa taifa.

Kitendo kile hakikuwa kizuri na kilitishia hata mechi kuvunjika kwa sababu viongozi wa  African Lyon wanasema walifanya kila kitu kwa kufuta sheria na kanuni hivyo walikuwa sahihi, na walisisitiza hata katika kikao cha kabla ya mechi walipeleka jezi zao na zikapitishwa na kwa ajili ya kuchezewa katika mechi ya baadae.

Kiukweli kitendo kile ambacho kilikosa majibu ya kueleweka hakikuwa kizuri na kileleta aibu katika soka letu, pia kinaweza  kuwakimbiza wadhamini wengine ambao walikuwa na interest ya kuja kuwekeza kwenye soka letu.

BAADA YA MECHI
Kutokana na kitendo kile nilijaribu kufuatiliwa na kutaka kujua kiundani kwanini imekuwa tatizo kwa African Lyon kuwa na mdhamini ambaye ni mshindani wa kibiashara na mdhamini mkuu wa ligi.

Katika kufuatiliwa kwangu nimekuja kupata taarifa za kuaminika kutoka baadhi ya viongozi wakuu wa vilabu vya ligi kuu kwamba mpaka sasa hakuna mkataba wowote halali wa kibiashara baina ya vilabu hivyo na kampuni yoyote juu ya udhamini wa ligi kuu ya Tanzania bara ambayo msimu huu ipo chini ya vilabu kupitia kamati ya ligi. Kwa maana katibu mkuu wa TFF Bwana Angetile Osiah amekuwa akitoa taarifa za uongo juu ya udhamini mpya wa Vodacom kwenye ligi kuu.

Ni kweli kwamba kumekuwepo au kulikuwepo na mazungumzo ya kati ya Vodacom na vilabu kupitia mwakilishi wao TFF, lakini mpaka sasa hakuna mkataba wa kisheria ulio halali baina ya pande mbili kwa maana hiyo ligi haina mdhamini rasmi. Hivyo taarifa anazotoa katibu mkuu wa TFF sio sahihi.

Mkataba huo sio halali kwa kuwa hakuna kiongozi wa timu yoyote aliyesaini mkataba huo wa udhamini na Vodacom. Ukweli ni kwamba TFF kupitia Angetile Osiah alikuwa kama mdhamini(Guarantor) katika majadiliano na utiaji saini wa mkataba, hivyo ilipaswa kwanza viongozi wa vilabu kupitia viongozi wao Mzee Said Mohamed na Wallace Karia wasaini kwanza ndio wampe Guarantor wao TFF aweke saini, lakini haikuwa hivyo na kwasababu wazijuazo wenyewe Angetile Osiah akatia saini kwenye mkataba kabla ya vilabu kufanya hivyo.

Je kwa sababu zipi, mdhamini wa kwenye mkataba akawa na haraka ya kuusaini mkataba kuliko wahusika halisi kabisa ambao ni vilabu au kuna 10% ya kuhakikisha dili la udhamini linaenda pale anapopataka? Majibu anayo mwenyewe.

KWANINI VILABU HAVIJASAINI MKATABA MPYA NA MDHAMINI WA LIGI?
Viongozi wakuu wa vilabu wanasema sababu kuu walizoshindwana mpaka sasa na mdhamini wa ligi aliyepita ni tatu tu.

1: Mdhamini kutaka apate upekee - yaani asiyewepo mpinzani wa moja kwa moja wa kibiashara katika issue nzima ya kutoa udhamini katika ligi, kwa shirikisho na vilabu pia. Vilabu vikatoa kauli ya pamoja kwamba ili mdhamini mkuu aweze kupata haki ya upekee inabidi a-double fedha anayota kwa  mwaka, jambo ambalo Vodacom walilikataa.

2: Fedha za udhamini: Kwa mujibu wa viongozi wa vilabu ni kwamba mdhamini wa ligi aliyepita alitoa ofa ya kutoa kiasi cha Billioni 1.6 kwa kila mwaka ndani ya kipindi cha miaka 3, lakini viongozi wa vilabu wakalipinga hilo kwa kutoa sababu kwamba lazima kiwepo kipengele cha ongezeko la thamaini ya fedha - kwa maana shilingi billioni ya mwaka huu haitakuwa sawa na thamani ya mwaka au miaka miwili mbele. Kwa maana hiyo wakaomba liwepo ongezeko la asilimia 10 ya fedha wanayopewa kwa kila mwaka.

3: Pendekezo la tatu ni kwamba mkataba uwe wa miaka miwili na si mitatu. Suala hili pia  likakataliwa.

Mapendekezo haya matatu ndio yaliyochangia uchelewashaji au kutokuwepo kwa mkataba wa udhamini wa ligi ulio halali kisheria.

NINI KINAFUATA
Kwa taarifa nilinazo ni kwamba viongozi wa timu za ligi kuu walikuatana jana jioni jijini Dar Es Salaam ili kujadili namna ya kuepukana na ukiritimba wa TFF na mikataba yao, na ikiwa kutatokea kampuni yoyote yenye  kutaka kuidhamini ligi kuu lazima suala ya 'exclusivity ' lisiwepo ama kuongeza kiasi cha pesa na kufikia walau shilingi za kitanzania bilioni tatu ili kuondoa aibu ambayo iliikumba soka ya Tanzania jumamosi.

Pia wakaafikiana kwamba ligi ya mwaka huu itaitwa "Ligi kuu ya Tanzania Bara" na sio vinginevyo, huku wakitoa kauli rasmi kwamba hawautambui mkataba wa udhamini na Vodacom kwa sababu sio halali kwa maana hakuna kiongozi yoyote wa klabu aliyetia saini mkataba huo.

Pia viongozi wa vilabu kwa pamoja wamesikitishwa sana na kitendo ilichofanyiwa African Lyon na kukilaani vikali.

No comments:

Post a Comment